TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATOKEO YA UDAHILI WA AWAMU YA PILI WA KOZI ZA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI KATIKA MKUPUO WA SEPTEMBA 2022/2023

BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (NACTVET)

This image has an empty alt attribute; its file name is NACTVET-logo.jpeg

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATOKEO YA UDAHILI WA AWAMU YA PILI WA KOZI ZA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI KATIKA MKUPUO WA SEPTEMBA 2022/2023

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linapenda kutoa taarifa kwa umma kwamba matokeo ya uchaguzi awamu ya pili kwa waombaji wa programu za afya katika mkupuo wa Septemba 2022/2023 yametoka rasmi leo tarehe 12 Septemba, 2022. Baraza lilipokea jumla ya waombaji wapya 3,659, ambao walifanya jumla ya maombi 4,607. Kati yao, waombaji wanawake ni 1,704 (46.6%) na wanaume1,955 (53.4%).

Jumla ya machaguo 4,121 (89.4%) yalikidhi sifa za kujiunga na program mbalimbali za afya na sayansi shirikishi. Jumla ya waombaji wapya 2,554 (69.8%) walikidhi sifa na kuchagualiwa kujiunga na program walizoomba. Kati yao wanawake ni 1,313 (51.4%) na wanaume 1,241 (48.6%) wamechaguliwa kujiunga na programu mbalimbali zinazotolewa na Vyuo 178 katika awamu hii ya pili. Waombaji wengine 267 (10.4%), wanawake 110 (41.2%) na wanaume157 (58.8%) waliokuwa na sifa hawakuchaguliwa katika machaguo yao kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ushindani na nafasi kuwa finyu kwenye Vyuo walivyoomba.

Pia, Baraza linapenda kuujulisha umma kwamba jumla ya waombaji 4,809 wenye sifa ambao hawakupata nafasi za masomo katika dirisha la awamu ya kwanza, wamechaguliwa awamu hii ya pili kwenye Vyuo walivyoomba awali. Kati ya hao, wanawake 2,409 (50.1%) na wanaume 2,400 (49.9%). Kuchaguliwa kwao kumetokana na kupatikana nafasi kwenye vyuo hivyo baada ya baadhi ya waliochaguliwa awamu ya kwanza kushindwa kuthibitisha iwapo watasoma kwenye vyuo husika.

Waombaji wote wanaweza kuangalia majibu yao kupitia kiunganishi bonyeza hapa kwa ajili ya kupata taarifa zaidi. Kwa wale waliofanikiwa kuchaguliwa, wanashauriwa kupakua fomu za kujiunga na kuwasiliana na Vyuo moja kwa moja kwa ajili ya kuthibitisha nafasi hizo. Baraza linawashauri waombaji wote ambao hawapo tayari kujiunga na Vyuo walivyopangiwa kufanya mawasiliano na Vyuo husika kwa maelekezo zaidi. Aidha,waombaji wote ambao hawakuchaguliwa wanatakiwa kufuata maelekezo yaliyopo kwenye kurasa zao za maombi (profile) ili kujaza machaguo mapya kwenye dirisha la tatu kuanzia tarehe 12/09/2022 hadi tarehe 23/09/2022. Matokeo ya uchaguzi wa awamu ya tatu yatatolewa tarehe 30/9/2022. Wanafunzi wataripoti chuoni kuanzia tarehe 3/10/2022 hadi tarehe 18/10/2022.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA KATIBU MTENDAJI

BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (NACTVET) 12/09/2022