TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUFUNGULIWA KWA DIRISHA LA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2023/2024

BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (NACTVET)

This image has an empty alt attribute; its file name is NACTVET-logo.jpeg

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU WAOMBAJI WA UDAHILI WA ASTASHAHADA NA STASHAHADA KWA MWAKA WA MASOMO 2023/2024

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linapenda kuufahamisha umma kuwa Udahili wa wanafunzi kwa Ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa kozi/programu zote zinazotolewa na Vyuo mbalimbali umefunguliwa rasmi kuanzia tarehe 21 Mei hadi tarehe 30 Juni, 2023 katika awamu ya kwanza.

Wahitimu wote wa Elimu ya Sekondari na Vyuo wenye sifa za kujiunga na kozi za Astashahada na Stashahada, wanashauriwa kufanya maombi yao kwa umakini ili kupata nafasi ya kujiunga kozi/programu wanazozipenda na ambazo wanatimiza vigezo/sifa za kujiunga nazo kwa mwaka wa masomo 2023/2024. Maombi ya kujiunga na kozi/programu mbalimbali yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.

Aidha, Waombaji wa programu za Afya na Sayansi Shirikishi – Tanzania Bara, wanapaswa kuwasilisha maombi yao kupitia Udahili wa Pamoja (Central Admission System – CAS) katika tovuti ya Baraza (www.nacte.go.tz).
Baraza pia, linawashauri waombaji, wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanaomba kwenye Vyuo ambavyo vimeorodheshwa kwenye Mwongozo wa Udahili kwa Mwaka wa Masomo 2023/2024 (Admission Guidebook for 2023/2024 Academic Year). Mwongozo huo unapatikana katika tovuti ya Baraza (www.nacte.go.tz).

Baraza linatoa rai kwa waombaji wote kuandika taarifa zao sahihi na kutunza taarifa watakazopatiwa na Baraza bila kumpatia mtu yeyote ili kuepusha usumbufu katika zoezi zima la maombi yao kujiunga na vyuo/ programu mbalimbali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (NACTVET)
21/05/2023